Health

Mazoezi kwa watu wazima huongeza uwezo wa kukumbuka


Ripoti ya utafiti iliyochapishwa katika jarida la Health Physiology na kuchapwa katika wavuti ya WebMD inadai kuwa watu wazima wenye tabia ya kufanya mazoezi ya kuendesha baiskeli au kujinyosha viungo vyao huongeza uwezo wa kukumbuka zaidi kuliko wale wasiofanya kabisa.

Utafiti huo unadai kuwa pamoja na kwamba kimuundo ubongo haufanani na misuli lakini kadri mtu anavyozeeka kuingia utu uzima, ufanyaji mazoezi husaidia kuimarisha uwezo wake wa kukumbuka na hata kufikiria mambo mapya.

Jambo la kutia moyo ni kuwa huna haja ya kufanya mazoezi mazito kwa vile mazoezi mepesi tu kama ya kunyoosha nyoosha viungo yanatosha kuleta kabisa matokeo ya kuridhisha.

Uchunguzi huo ambao ulihusisha watu wazima waume kwa wake waliokuwa wakiendesha baiskeli au mazoezi ya kunyoosha viungo kwa muda wa saa mbili kwa wiki kwa muda wa miezi sita ulionesha kuwepo kwa maendeleo makubwa katika uwezo wao wa kukumbuka mambo na hata kufikiria mambo mapya.

Mmoja wa watafiti hao Kirsten Hotting kutoka chuo kikuu cha Hamburg, Ujerumani anasema kuwa mtu anayefanya mazoezi ya aina mbalimbali kwa pamoja ana uwezekano wa kupata matokeo mazuri zaidi.

Ripoti hii inaweza kutafsiriwa kama changamoto kwa watu walio katika nafasi mbalimbali za kutoa maamuzi kiuongozi kuwa tabia ya ufanyaji mazoezi inaweza kuimarisha sana uwezo wao wa kukumbuka mambo na kufikiria mambo mapya, na hivyo kuzidi kuongeza tija katika utendaji wao wa kila siku. Aidha hii ni changamoto hata kwa watu wengine kuanzisha utaratibu wa kujifanyia mazoezi mepesi kwa ajili ya kuimarisha afya ya akili na mwili kwa ujumla.

Ripoti ya utafiti huu inapatikana katika Jarida la Health Psychology


Usumu/Maambukizi kwenye chakula (Food poisoning): Yaweza kuzusha tafrani


i mara chache tumewahi kushuhudia au kusikia mtu au kundi la watu likiugua ghafla baada ya kula chakula katika mkusanyiko au sherehe. Bila shaka nawe ni mmojawapo wa waliowahi kukumbwa na hali hii. Aidha tumewahi pia kusikia au kushuhudia hata baadhi ya watu wakiamini kulishwa sumu baada ya kula chakula katika shughuli au sherehe fulani. Hali hii imewahi kuzusha tafrani na sintofahamu miongoni mwa wanajamii kwa vile si wengi wanaofahamu hasa chanzo cha hali hiyo.

Lakini usumu au maambukizi katika chakula (food poisoning) ni nini hasa?
Food poisoning ni hali ya kuchafuka kwa chakula kunakotokana na uwepo wa vimelea mbalimbali kama vile bacteria, virusi, au parasites au sumu zao ndani yake. Hali hii hutokea wakati unapokula chakula au kunywa vinywaji/maji yaliyochanganyika na vimelea hawa hususani vya bacteria wa jamii ya Staphylococcus au Escherichia coli (E. coli).
Ieleweke kuwa food poisoning haimaanishi sumu inayowekwa na mtu/watu kwenye chakula bali hutokana na vijidudu vya magonjwa mbalimbali kama vile bacteria.

Vihatarishi vyake
Kwa kawaida food poisoning hutokea zaidi baada ya kula vyakula vilivyoandaliwa kwenye mikusanyiko kama vile cafeteria za shule au kazini, kwenye misiba, matanga, hitma, maulid, ngoma, harusi, mahoteli, na mikusanyiko mingine yeyote ambayo inahusisha ulaji wa chakula cha pamoja; ambapo mtu mmoja au kundi la watu hupatwa na usumu huo na kuwa wagonjwa.

Watoto wadogo chini ya mwaka mmoja pamoja na wazee ni miongoni mwa makundi ya watu wanayoongoza kuwa katika hatari ya kuathirika zaidi na tatizo hili. Wengine ni pamoja na watu wenye matatizo ya kiafya kama vile magonjwa ya figo au kisukari, wenye upungufu wa kinga ya mwili, na wasafiri wanaotembelea maeneo yanayojulikana kuwa na vimelea wanaosababisha hali hii kwa wingi.

Visababishi
Kama ilivyotangulia kuelezwa hapo awali, food poisoning husababishwa na sumu inayotokana na vimelea vya bacteria, virusi, au parasites. Vimelea hawa hujumuisha bacteria jamii ya
• Clostridium botulinum wanaosababisha usumu unaoitwa botulism
• Campylobacter wanaosababisha uambukizi kwenye utumbo mdogo kuharisha na kutapika
• Vibrio cholera wanaosababisha kipindupindu
• E. coli ambao pia husababisha uambukizi katika utumbo mdogo, kuharisha na kutapika
• Bakteria wengine ni pamoja na Staphylococcus aureus, Salmonella, Listeria na Shigella ambao husababisha kuharisha damu, na aina fulani ya bacteria wanaopendelea kuishi kwenye magamba ya samaki.

Vimelea wa sumu huingiaje kwenye chakula?
Kuna njia kadhaa ambazo hutumiwa na bacteria kuvamia chakula na hatimaye kuzalisha sumu zao na hivyo kukichafua. Njia hizo ni pamoja na
• Maandalizi pamoja na upikaji mbaya wa chakula
• Maji yasiyo safi na salama yanaweza kuwa na kinyesi cha binadamu au wanyama ambacho huwa kimebeba vimelea hawa
• Nyama inapogusana na utumbo/matumbo ya wanyama yenye vimelea hawa wakati wa kuchinja, kuchuna ngozi na kuandaa nyama

Aidha mtu anaweza kupata food poisoning baada ya kula au kunywa:
• Chakula kilichoandaliwa na mtu mwingine au yeye mwenyewe bila kusafisha vema mikono yake
• Chakula kilichoandaliwa kwa kutumia vyombo vichafu kama vile masufuria machafu, majungu, vijiko, visu, vikombe, sahani au vyombo vingine vinavyotumika kuandaa au kulia chakula.
• Vyakula vya jamii ya maziwa, jibini, mtindi ambao umewekwa kwenye friji kwa muda mrefu bila uangalizi wa kutosha.
• Vyakula vilivyohifadhiwa kwenye jokofu katika joto lisilo sahihi bila kuvipasha tena moto
• viporo visivyohifadhiwa vema
• samaki wabichi/wasioiva au kamba kochi
• matunda au mboga mboga mbichi zisizooshwa vizuri
• saladi isiyoandaliwa vema
• nyama isiyoiva vema au mayai mabichi
• maji kutoka katika bomba bila kuchemsha hususani kama limepasuka

Zipi ni dalili za food poisoning?
Dalili za mtu mwenye food poisoning hutegemea na aina ya vimelea wanaosababisha hali hii. Kwa kawaida, vyanzo vingi vya food poisoning huwa na dalili zinazojitokeza ndani ya saa 2 mpaka 6 tangu mtu anapokula chakula chenye usumu. Baadhi ya dalili za ujumla ni pamoja na
• maumivu ya tumbo. Tumbo huwa kama linakata au kusokota.
• Homa na kujihisi baridi
• Kuumwa kichwa
• Kichefuchefu na kutapika
• Kuharisha, kulingana na chanzo mtu anaweza kuaharisha majimaji au kuharisha damu
• Mwili kuwa dhaifu na kulegea. Ulegevu wa mwili unaotokana na usumu wa botulism waweza kuwa mbaya sana kufikia kusababisha mtu kushindwa kupumua sawasawa na hatimaye kifo.

Vipimo na uchunguzi
Mara unapofika kwa hospitali, daktari pamoja na kukuuliza maswali ili afahamu vizuri historia na chanzo cha ugonjwa, pia atakupima ili kutambua viashiria vingine kama vile upungufu wa maji mwilini au maumivu ya tumbo. Daktari atakuuliza kuhusu vyakula au vinywaji ulivyokula na kunywa saa kadhaa zilizopita, kama uliandaa mwenyewe au la, ulikuwa au kunywa wapi, kama kuna wengine wenye dalili kama zako, dalili nyingine kama kuharisha, kutapika, vichefuchefu, maumivu ya tumbo, homa au dalili nyingine kama zilivyotajwa hapo juu.

Daktari pia anaweza kushauri ufanyike uchunguzi kama wa damu, mkojo, choo, matapishi, au masalia ya vyakula ili kutambua chanzo cha ugonjwa wako. Hata hivyo ieleweke kuwa wakati mwingine vipimo hivi vinaweza kushindwa kuthibitisha kwamba ugonjwa wako unatokana na kuwepo kwa usumu kwenye chakula. Baadhi ya wagonjwa wanaoharisha damu wanaweza kuhitaji kufanyiwa vipimo zaidi ili kutambua chanzo cha kuharisha damu ili kujiridhisha kuwa hakuna uhusiano na food poisoning.

Matibabu
Wagonjwa wengi wa food poisoning kwa kawaida hupona kabisa baada ya siku chache tangu kujitokeza kwa dalili. Jambo la msingi ni kuhakikisha unaendelea kula na kunywa vinywaji au maji ya kutosha ili kurejesha kiasi chochote cha maji kitakachopotea kutokana na kuharisha au/na kutapika.

Haishauriwi kula vyakula vigumu mpaka kuharisha kutakapokoma, na jiepushe kula vyakula vya jamii ya maziwa (maziwa, mtindi) ili kupunguza uwezekano wa kuharisha zaidi, wakati huo huo kunywa maji ya kutosha au vinywaji vingine kwa wingi.

Watoto wadogo ni vema wapewe maji yenye madini maalum ya ORS au kama hayapatikani, maji yenye mchanganyiko wa chumvi na sukari hufaa sana. Wagonjwa hususani watoto wanaoharisha na kutapika na ambao hawawezi kunywa maji wala vinywaji kwa sababu ya kutapika hawana budi kutibiwa kwa kutumia drip (i.v. fluids) ili kurejesha maji yaliyopotea.

Mara nyingi, matibabu ya food poisoning hayahusishi utumiaji wa dawa za jamii ya antibiotics isipokuwa mara chache sana daktari wako anaweza kushauri utumie dawa hizo hususani kama kunaambatana na kuharisha damu.

Nini cha kutarajia kwa mtu aliyepatwa na food poisoning?
Kwa kwaida watu wengi wenye kupatwa na hali hii hupata nafuu kamili ndani ya saa 12 mpaka siku mbili; ingawa wapo baadhi ambao hali zao zinaweza kuwa mbaya sana. Ni mara chache food poisoning husababisha kifo lakini kama mgonjwa anaharisha sana na kutapika bila kutibiwa, kifo kinaweza kutokea kwa sababu ya upungufu mkubwa wa maji mwilini.

Nini madhara ya hali hii?
Madhara yaliyozoeleka zaidi ya hali hii ni upungufu wa maji mwilini unaotokana na kutapika na kuharisha kupita kiasi bila kurejesha maji yanayopotea.
Madhara mengine hutegemeana na aina ya bacteria anayesababisha ugonjwa huu. Bacteria wengine husababisha madhara kama vile magonjwa ya figo, matatizo ya kutokwa damu bila kukoma, magonjwa ya viungo vya mwili, magonjwa ya mfumo wa fahamu, na madhara katika moyo.

Kinga ni bora kuliko tiba
Kujikinga ni bora kuliko kusibiri mpaka tatizo litokee. Unashauriwa kuepuka kula vyakula ambavyo ubora na usafi wake unatia shaka. Aidha epuka kunywa vinywaji au maji ambayo si safi na salama pamoja na kuacha kula nyama au samaki wasiopikwa vizuri.

Unashauriwa kwenda hospitali haraka iwapo utaona damu au usaha katika kinyesi chako, kinyesi kimekuwa cha rangi nyeusi, tumbo linazidi kusokota hata baada ya kujisaidia, kujihisi dalili za kukaukiwa maji mwilini kama vile kiu, kizunguzungu au kujihisi kichwa chepesi, kuharisha pamoja na homa kali, moyo unakwenda kasi au una dalili nyingine za tatizo hili.

Kukosa Usingizi Husababisha Upungufu wa Homoni ya Testosterone


Mnamo mwaka 2007, watafiti nchini Marekani walifanikiwa kutoa ripoti inayojaribu kuhusisha ukosefu wa usingizi na upungufu wa homoni ya testosterone miongoni mwa wanaume watu wazima.

Kwa kawaida kiwango cha homoni ya testosterone hupungua kadiri mwanaume anavyozidi kuwa mtu mzima, na kwa baadhi ya wanaume, kupungua huku kwa testosterone huweza kusababisha ulegevu wa mwili, kukosa hamu ya ngono na hata kuvunjika mifupa ya mwili.

Watafiti wanasema kuwa, wapo baadhi ya wanaume walio kwenye miaka 80 bado huweza kuwa na kiwango cha juu cha testosterone sawa na kile kinachopatikana kwa wanaume vijana. Hata hivyo sababu kubwa inayofanya kuwepo na utofauti katika viwango vya testosterone miongoni mwa rika hizo mbili bado hazieleweki sawasawa, ingawa watafiti wanasema kuwa ukosefu wa usingizi miongoni mwa watu wazima na wazee unaweza kuwa chanzo kimojawapo cha kuwepo kwa hali hiyo.

"Matokeo ya utafiti wetu yanaongeza uwezekano kuwa wanaume watu wazima na wazee ambao hupata muda mfupi sana wa kulala nyakati za usiku huwa na kiwango kidogo sana cha homoni ya testosterone wakati wa asubuhi," anasema mtafiti Plamen Penev, wa kutoka Chuo Kikuu cha Chicago, nchini Marekani.

Wakati wa utafiti, wataalamu waliofanya uchunguzi huo walipima kiwango cha homoni ya testosterone katika damu kila asubuhi cha wanaume watu wazima wenye umri kati ya miaka 64 na 74 waliojitolea kushiriki kwenye utafiti huo. Aidha, mtindo wao wa kulala pamoja na kupata usingizi pia vilichunguzwa kila siku kwa muda wa wiki nzima.

Matokeo ya uchunguzi huo yalionesha kuwa kiasi cha usingizi walicholala kilikuwa na uhusiano wa karibu sana na kiwango cha testosterone katika damu wakati wa asubuhi. Wale waliopata usingizi mzuri na kwa muda mrefu (walau saa nane) walikuwa na kiwango kikubwa cha testosterone wakati wale waliopata usingizi wa kubabaisha (saa nne) walikutwa na kiwango cha chini cha homoni hiyo. Wastani wa muda wa kulala ulikuwa masaa sita.

"Pamoja na kwamba matokeo ya utafiti huu yanaonesha kuwa urefu wa muda wa kulala wa mtu waweza kuwa kiashiria cha mabadiliko ya homoni katika mwili yanayohusiana na umri, matokeo ya utafiti huu yanatoa tu picha ya nini kinachotokea mwilini kama mtu asipopata usingizi wa kutosha. Hata hivyo, tafiti zaidi zinahitajika ili kuthibitisha umuhimu wa uhusiano kati ya usingizi na mabadiliko ya homoni katika mwili," anasema Dr. Penev.

Wataalamu wa masuala ya afya ya usingizi wanashauri watu wazima kupata wastani wa angalau saa saba mpaka nane za kulala kila usiku ili kuwa na afya bora. Ripoti kamili ya matokeo ya utafiti huu inapatikana katika toleo la mwezi April, 2007 la jarida la afya la Sleep.


No comments:

Post a Comment

 

Sample text

Sample Text

Sample Text

 
Blogger Templates